Kwa kutumia mifano jadili istilahi muhimu katika tamthiliya ya tanzia.
Kwa
kutumia mifano jadili istilahi muhimu katika tamthiliya ya tanzia.
MPANGO KAZI
Katika
kazi hii, tumelenga kufafanua dhana ya tamthiliya, dhana ya tanzia pamoja na
istilahi za msingi katika tamthiliya ya tanzia. Pia kazi yetu imegawanyika katika sehemu kuu tatu
yaani Utangulizi, kiini cha swali, na hitimisho.
Katika
sehemu ya utangulizi tumejadili dhana ya tamthiliya na tanzia kwa kurejea
wataalamu mbalimbali kama vile, TUKI, (2004), Mlama, (1983:203) katika dhana ya
tamthiliya. Katika dhana ya tanzia tumeweza kuwatumia wataalamu kama vile Semzaba,
(1997)
Katika
sehemu ya pili ambayo ni kiini cha swali hapa tumeweza kujadili istilahi mbalimbali za msingi katika
tamthiliya ya tanzia.
Vilevile
katika sehemu ya mwisho ambayo ni hitimisho tumeweka mawazo ya jumla ya kazi
yetu.
UTANGULIZI.
Maana
ya tamthiliya.
Kwa
mujibu wa TUKI, (2004). Tamtiliya ni utungo wa kisanaa ambao huweka wazo fulani
katika matendo na mazungumzo.
Tamthiliya
ni sanaa ya maonyesho, sanaa ambayo huwasilishwa, ana kwa ana, tukio fulani kwa
hadhira kutumia usanii wa kiutendaji. Mlama, (1983:203).Hivyo kwa ujumla
tunaweza kusema kwamba tamthiliya ni utungo au mchezo wa kuigiza matendo au
mawazo fulani yaliyopo katika jamii ambapo huwa na majibizano baina ya watu wa
pande mbili wanaweza kuwa wawili au zaidi, tamthiliya huweza kuigizwa jukwaani
pia huweza kuandikwa tu bila kuyaigiza matendo jukwaani na kubaki kusomwa
pekee.
Dhana ya tamthiliya ya tanzia.
Tanzia
ni kinyume cha ramsa kwa maana kuwa hutumika kuonesha kuanguka na kushindwa kwa
mhusika maarufu, mbabe au shujaa atokaye katika tabaka la juu yaani mtu mwenye
nasaba bora. (Mutembei, 2005 katika mhadhara a SW 234).
Kama
ilivyo kwa ramsa, tanzia ilianza katika miungu ya kidini katika sherehe ya
kumhusu Dionsius. Wachezaji na waigizaji walivalia na kuonekana kama mbuzi.
Wakiimba nyimbo zilizohusu anguko la shujaa huyo.
Tamthiliya
ya tanzia ni tamthiliya yenye huzuni inayogusa hisia za watazamaji au wasomaji
kiasi cha kuogopesha na kumwonea huruma mhusika mkuu ambaye hupatwa na janga. Mhusika
mkuu huwa ni mbabe, au shujaa atokaye tabaka la juu mtu wa nasaba bora na
ambaye huwa anajaribu kubadilisha hali yake na jamii inayomzunguka.
Katika hatua yake hiyo hujikuta amefanya kosa au amefanya uamuzi usio sahihi,
uamuzi ambao husababisha anguko lake. Semzaba,(1997).
Kwa
ujumla tunaweza kusema kuwa tanzia ni aina ya tamthiliya ambayo huwa na suala,
matendo na malengo ya dhati. Aristotle aliona utanzu huu kama “mwigo au uigaji”
wa tendo ambalo linaudhati, uaminifu, ubora na ukuu Fulani. Kwa mujibu wa
mtaalamu huyu tendo hilo lazima liwe na uwezo wa kuathiri mtazamaji na kufanya
waingiwe na huzuni au kihoro .Pamoja na
kuwa na uwezo wa kuziteka hisia za woga au huzuni katika kile alichokiiita
mtakaso hisia. Tanzia aliyoikusudia Aristotle iliwahusu wahusika wakwezwa kama
wafalme na malkia na wengine.
Sehemu ya pili.
Hapa
tumejadili istilahi za msingi katika tamthiliya ya tanzia kama ilivyojadiliwa
na wataalamu mbalimbali kama vile Mutembei, (2005). Na wengine.
Istilahi
katika tamthiliya ya tanzia.
A. PERIPETEIA
Peripeteia hili ni neno
la Kiyunani ambapo mtu na kwa muktadha wetu, mhusika katika tamthiliya hubadili
nia iliyopaswa kuwa njema na kurudisha kinyumenyume dhamiri iliyokuwa iwe na
matokeo mazuri. Mhusika hufanya tukio au kuchukua hatua ambayo humtoa katika
usalama na kumwingiza matatani. Kwa mfano, unapokuwa na nia ya kwenda kusali
kanisani au kuswali msikitini, halafu ghafla unabadili nia na kwenda kwa
mchumba wako. Balaa unalolipata kule kwa mchumba wako linatokana na wewe
kubadili nia yako ya awali ya kwenda kwenye ibada. Na hii ndiyo Peripeteia.
B. ANAGNORISIS
Anagnorsis
hii ni dhana nyingine inayoenda sambamba na Peripeteia. Balaa ya mhusika mkuu
kubadili nia yake ya awali na kuamua kwenda upande wa pili au kuamua kufanya
tukio jingine ambalo bila yeye kujua litamwingiza matatani, inafikia wakati
sasa anatambua ah! Nimefanya uamuzi ambao sio sahihi. Huko kugundua ndiyo
Anagnorsis yaani tukio la mwanzo la kupata ufahamu. Mhusika mkuu hutambua kuwa
amejiingiza matatani kutokana na hatua moja au nyingine. Kwa mfano, unapoamua
kuacha shule, ambayo ndiyo sehemu pekee ya kupanua upeo wa maarifa na kuanza
kutafuta vibarua kwa shida kwasababu tu ulidanganywa. Pale unapogundua oh!
Kumbe umekusea kuacha shule kwa kuona ugumu unaoupata, hiyo ndiyo Anagnorsis.
Kwa
mfano katika tamtiliya ya Mashetani, baada ya binadamu kumuua shetani anaanza
kujiuliza maswali fulani ya kujuta na ansema laiti angefuata ule uamuzi wake wa
mwanzo.
Kumbe
basi Peripeteia unabadili nia na kuingia
upande wa pili, na katika upande wa pili unagundua umekosea (anagnorsis)
C. HAMARTIA
Hivyo baada ya kubadili
nia (Peripeteia) na kugundua kuwa amekosea (anagnorsis), mhusika mkuu hufanya
kosa fulani na kosa hilo ndio Hamartia. Mhusika hukosea sio kutokana na kosa la
kimaadili, bali zaidi kosa la kiutendaji au kiufundi, yaani mtu kulenga vibaya
shabaha na kupiga sehemu tofauti na kuzua balaa. Kwa mfano unapotaka kumuua
nyoka, badala ya kumpiga kichwa unampiga mkia au unampiga kidogo. Matokeo yake
atakugonga wewe na unakuwa umepatwa na balaa. Hata Mfalme Edipode anapogundua
kuwa amemuua baba yake na kumuoa mama yake anaamua kujitoboa macho.
Kosa la namna hii
hujutiwa sana na mhusika mkuu kwa sababu huwa ni kosa la kiuamuzi, dhambi au
matendo maovu na kosa hili ndilo husababisha anguko au kifo cha mhusika mkuu.
D. KATHARSIS (UTAKASO)
Ni
tukio au hali ambapo hisia za hadhira au mhusika hubadilika kabisa kutoka
katika hisia za masikitiko, huzuni, majonzi au furaha kuu na kuwa kinyume
chake. Katika istilahi hii ni kuwa Ili mtu ajiondoe katika hamartia hupaswa
kujitakasa na kujitakasa ni kwa kihisia. Tukio hili hujulikana kama Katharsis. Kwa
mfano katika tamtiliya ya Mashetani,
mwisho kabisa Juma anakataa kubadilisha nafasi yake na kuwa binadamu na Kitaru
anasikitika sana kuwa alidhulumiwa sana kwa kucheza nafasi ya binadamu, na
alitaka kujitakasa kwa kucheza nafasi ya shetani na yeye, lakini bahati mbaya
Juma alikataa.
Ni matukio au matendo ya kujitapa
kupita kiasi au kupindukia na kuonesha kuwa anayejitapa ametia chumvi mno hata
kukiuka uhalisia ulivyo. Kujitapa huwa zaidi kuelekeza kukashifu au kudharau
miungu au Mungu. Hii hasa huwapata watu wenye uwezo fulani (wanasayansi na
wasomi pia) au wenye vyeo na mamlaka. Pale wanapokosa unyenyekevu na kujiona
bila wao hakuna linaloweza kufanyika. Kutokana na hali hii, hubris huonekana kuwa
kama dhambi maana huvuka mipaka ya hali ya kawaida. Kutokana na kutapa huko,
husababisha anguko na mateso badaye.
Kwa
mfano katika tamtiliya ya Mashetani uk. 9, wako
wapi waliokuwa wakijitapa? Binadamu anacheka hadi kicheko kinamlevya, na hii
ni baada ya kudhani kamuua shetani kumbe wala hakuwa amemua.
Hubris
inahusishwa na miungu na kujitapa huku baadaye mhusika huyo lazima apate matatizo.
Kujitapa huku kiasi wakati mwingine huwa ni kwa sababu anayejitapa huwa hana
uelewa wa kutosha au pengine ni kujisikia kulikopita mipaka.
F. NEMESIS.
Nemesis alikuwa malaika
wa Kigiriki na alikuwa akiongeza na kupunguza mambo mbalimbali ikiwa hali ni wingi
kupita kiasi, hupunguza na ikiwa ni kidogo mno huongeza. Kama ulikuwa ukijitapa
kwa sababu ya uwezo wako mkubwa basi unapunguzwa.
Kutokana na hali hii,
anayesemwa ana hubris hujikuta uso kwa uso na Nemesis yaani kupata
kilichostahiki kwa uwiano, kiwe kizuri au kibaya.
Kwa mfano huko
Marekani, kupigwa kwa Pentagon, Marekani ilikuwa ikijitapa sana hadi ikakufuru
kwamba hakuna vita iliwahi fanyika nchini humo. Baada ya pigo hilo Marekani
ikaweka uwiano, yaani kwenye uwiano sawa na nchi zingine (ikatoka kwenye
kujisifu kuwa nchi isiyoguswa).
HITIMISHO.
Hivyo basi tunaweza kusema kuwa tamthiliya ya tanzia huweza
kutokea kutokana na kuwepo kwa misingi mbalimbali kama vile kuamsha hisia za woga na huruma
miongoni mwa hadhira, Shujaa katika tanzia lazima awe mtu mwema, sura nzuri, umbo zuri
ili yanayomtokea yasitarajiwe vilevile wasomaji au
watazamaji huonesha
kuumia, kusikitika, kutokana na anguko la shujaa ambalo huja kutokana na uamuzi
wake au kosa lake mwenyewe kadri mtu anavyoonekana mwema au mzuri wa umbo.
MAREJEO.
Mohamed, S. A. (1999) Uhakiki wa tamthiliya. Historian a
maendeleo yake. Nairobi: Jomo
Kenyatta foundation.
Mlama, (1983).Utunzi wa tamthiliya katika mazingira ya Tanzania. Dar es salaam:
TUKI.
Mtembei, A. (2005).
Semzaba, E (1997). Tamthiliya ya Kiswahili. Dar es salaam: O.U.P.
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi Wa
Kiswahili.
Wafula, R.M. (1995) Kunga za nathari za Kiswahili, tamthiliya, riwaya na hadithi fupi.
Nairobi: East Africa Educational
publishers.
Comments