Uhakiki wa tamthiliya ya nguzo mama kwa kutumia nadharia ya saikochanganuzi
UTANGULIZI
Kazi hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu hizo ni utangulizi, kiini na hatimaye hitimisho. Katika utangulizi tumeweza kufafanua maana ya nadharia kwa kuwarejerea wataalamu mbalimbali ambao kwa kiasi kikubwa wameelezea vizuri maana ya nadharia. Wataalamu hao ni kama vile Masamba (2009), Sarantakos (1997), Martin E. Amin (2005). Lakini pia katika kiini tumeweza kujikita moja kwa moja na swali letu jinsi linavyotaka kuwa tutumie nadharia ya saikochanganuzi ili kuhakiki tamthiliya ya NGUZO MAMA. Hivyo katika sehemu hii ya kiini tumeweza kuonesha jinsi gani nadharia hii ya saikochanganuzi ilivyojidhihirisha kwenye kitabu cha NGUZO MAMA kutokana na wahusika mbalimbali kama vile Bi moja, Bi pili, Bi tatu, Bi nne, Bi tano, Bi sita, Bi saba, Bi nane na wahusika wengineo kama chizi. Hivyo basi katika kazi yetu tumeweza pia kuhitimisha kazi kwa kutoa mawazo kuwa ni jinsi gani wanawake wa patata wameweza kupambana vikali dhidi ya kuinua NGUZO MAMA kwa kuanzisha miradi mbalimbali pia na vikundi mbalimbali ambavyo kwa namna moja ama nyingine viliweza kusaidia kuinua NGUZO MAMA. Kwa utangulizi huu kazi yetu tunaianza kuichambua kama ifuatavyo kwa kutumia kitabu cha NGUZO MAMA;
Maana ya nadharia.
Masamba (2009:63) anasema, Nadharia ni kanuni, taratibu na misingi ambayo imejengwa katika muundo wa kimawazo kwa madhumuni ya kutumiwa kama kielelezo cha kuelezea jambo.
Sarantakos (1997:9), pia amefasili nadharia ni kama jambo linalofanywa na kuthibitishwa kwa uhakika au kwa utaratibu maalumu kwa njia ya utafiti kwa ajiri ya kuelezea jambo Fulani katika jamii.
Martin E. Amin (2005:10), anasema nadharia ni jumla ya mambo yote ambayo mtafiti amekusudia, kuelezea, kuchambua, kuelewa, au hata kutabiri jambo fulani kwa utaratibu maalumu.
Hivyo basi kwa ujumla wake nadharia huchukuliwa kama dira au mwongozo wa kumuongoza mtafiti au mchambuzi kuelezea jambo fulani kwa mtazamo unaotarajiwa kuwa ni imara zaidi kuliko mitazamo mingine.
Lakini pia nadharia ya saikochanganuzi 1896 mwasisi wake ni Sigmund Freud raia wa Australia, mtaalamu huyu alikuwa ni tabibu wa magonjwa ya akili, alifanya uchunguzi wa nafsia, alichunguza sana hasa sehemu ya nafsi iliyofichika yaani ung’amuzi bwete ili kujua asili ya tatizo kwa mgonjwa husika, alieleza kuwa ung’amuzi bwete ni sehemu ya akili ya binadamu ambayo huhodhi fikra, mawazo, hofu na mitazamo hasi ambayo haiwezi kukubalika na jamii, hofu na mawazo hayo hujitokeza katika ndoto.
Freud anafananisha fasihi na ndoto kwa kuwa riwaya, tamthiliya na ushairi ni kazi bunifu, kazi hizi zinashabiri ndoto. Usanii ni ruya, jozi zinazoashiria matumaini na matamanio ya mwandishi.
Freud anaiona kazi ya fasihi maudhui yake, mtindo wake, na wahusika wake kuwa ndoto inaweza kumuliwaza anapoipitia. Vitengo hivi vya fasihi humuathiri msomaji kiukweli licha ya kwamba anayoyasoma ni ya kubuni.
Imani nyingine ya Freud kuhusu fasihi inatokana na mitaala yake miongoni mwa wagonjwa wenye matatizo yanayohusiana na muundo wa jamii. Kwake Freud, mwiko wa kijamii unaowapinga wanawake na wanaume kujamiana wanavyotaka hutegemea silika zao kuwa ni kilele cha juu cha ukandamizwaji. Hapo ndipo dhana ya uanakama invyofikiliwa na Freud na kujitokeza katika kazi ya fasihi, (Wamitila 2003).
Tamthiliya ya nguzo mama ni kazi ya sanaa ya fasihi ambayo imeandikwa na Penina Mhando kwa ustadi mwingi na inamulika changamoto zinazomkumba mwanamke katika baadhi ya jamii zetu. Kwa sababu binadamu ni kiumbe wa kufikiri na kutunga mikakati ambayo imewekwa na akina mama ili waweze kukabiliana na changamoto hizo. Hivyo basi wajibu wetu kwenye kazi hii na kuchanganua na kuchambua Tamthiliya hii kwa kutumia nadharia ya saikochanganuzi. Katik Tamthiliya hii ya Penina Mhando ni miongoni mwa kazi ambazo zimechapishwa ili kuonyesha juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa tangu mwaka 1975 kuwakomboa wanawake kutoka katika ukandamizwaji na udhalilishwaji kupitia asasi mbalimbali za kijamii kama vile ndoa na utamaduni.
Ufuatao ni uhakiki wa tamthiliya ya nguzo mama kutokana na nadharia ya saikochanganuzi;
Taashira ni nini?
Taashira ni ishara au alama maalumu zitumikazo katika jamii kuwakilisha kundi fulani katika jamii. Mawazo yaliyo katika ung’amuzi bwete yanaweza kuwasilishwa katika ndoto, mitelezo ya kauli ambavyo vyote hubanwa kwenye ung’amuzi bwete. Hapa lazima taashira hizi zichambuliwe ili maana halisi iliyofichika ipatikane. Ubanaji unahusu kubana ujumbe uliopo Kwa namna iliyokubalika na uchanganuzi wa akili ya binadamu. Ubadilishaji Kwa upande wake unahusisha ugeuzaji wa yaliyomo katika ndoto na kuwasilishwa kwa njia tofauti.
Namna tatu za ung’amuzi bwete ni taashira, ubanaji na ubadilishaji. Katika tamthiliya ya nguzo mama kuna hali ya utabaka ambayo imejitokeza kabla ya igizo kuanza kwenye jukwaa. Kibwagizo cha wimbo klilisikika ndipo mwanamke aliyejulikana Kama Bi moja aliyekuwa amevaa kimwambao akatokezea na kuelekea kwenye sanamu yenye maandishi “NGUZO MAMA” Kibandiko hiki ni taashira ya kuleta umoja wa wanawake, matamshi ya Bi moja yanatupatia picha kuhusu mawazo yake ya tabaka na mazingira alimotoka.
Kisha Bi pili aliingia na maelezo tuliyopata kumuhusu mkulima ambaye ni mwenyeji wa bara. Kulingana na usemi wake ilidhihirika kuwa alitoka kijijini kwenye familia kubwa (watu wengi)
Hatimaye Bi tatu aliingia huku amevaa vitenge vya kizaire. Huyu alionekana mwenye uwezo (tabaka la juu) kwani aliyoyapendekeza ni kupamba NGUZO MAMA ni ya thamani kama vile mabenzi na mavolvo (aina ya gari za kifahari). Wahusika hao walishirikiana isipokuwa ni kwa muda mfupi kujaribu kuinua NGUZO MAMA.
Mitazamo tofautitofauti kuhusu wazo linaloibuka
Msimulizi: Moyoni walijiwazia pengine wazi walijisemea imeandikwa NGUZO MAMA yao hao wabeba wana, waachieni wenyewe mambo wajitengenezee. Kwani maendeleo ya Patata si ya wake na waume. (uk. 8)
Wanawake walijaribu kuisimamisha nguzo mama kutokana na mitazamo tofautitofauti.
Bi nne aliingia amevaa na kilemba na akatoa mapendekezo ili kupata uhuru wao wafanye mikutano na kutoa maazimio.
Bi tano aliingia na miondoko ya ngoma za madogori.
Bi sita aliingia na miondoko ya kikahabana amevalia kikahaba.
Bi saba aliingia na kutoka bila kusema chochote.
Msichana alikuwa anasikia sauti kila upande zina mwito, “njoo huku” kabla hajaenda taswira yake mtoto wa kike anapewa majukumu mengi ambayo humuathiri katika masomo yake.
Bi nane alikuwa msomi aliingia kama wengine na kutokuwa na umoja na mshikamano ndio kizingiti cha kuzuia uhuru wa wanawake usipatikane.
Bi nane alitoa mapendekezo na ushauri ili nguzo mama iweze kusimamishwa kwa lazima waivute kwa pamoja. Kamba inaashiria umoja na mshikamano. Hivyo wazo la Bi nane lilipingwa vikali sana na Bi nne ambaye alikuwa na fikra kwamba mamlaka yake yalikuwa hatarini.
Bi nne: alikuwa wapi wakati NGUZO MAMA ilitolewa na wala hakuonekana kwenye harakati za maandamano.
Msimulizi alitabiri kuwa zogo litatokea kwa sababu kila mtu afanya lake akiambiwa lile afanyalo, (uk. 17)
Bi pili aliamua kupika pombe na kuiuza kilabuni ili apate pesa. Yeye alidhani NGUZO MAMA haikusimama kwa sababu ya pesa.
Bi moja alikuja na wazo zuri la kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mapambo.
MISINGI YA NADHARIA YA SAIKOCHANGANUZI.
Msingi wa kwanza ni kuangalia uwezo na udhaifu wa binadamu katika kuzikabili hali ngumu za kimaisha.
Msingi huu katika nadharia hii ni muono wa binadamu au jamii nzima katika jamii yao ni jinsi gani wanaikabili hali ngumu za kimaisha. Katika kitabu cha NGUZO MAMA ukurasa wa 52 hii imejidhihirisha pale wanawake wa kijiji cha patata wanapoamua kuanzisha miradi ya kiuchumi ili kuinua NGUZO MAMA.
“……….Miradi tutatilia mkazo, miradi ya kila aina, vilabu vya pombe, maduka ya Khanga, ushirika wa kushona, kupika na mengine mengi…..uk 52.
Pia hii imejidhihirisha pale Bi pili alipoamua kuanzisha kilabu cha pombe ili kuweza kujikomboa kwenye maisha magumu kama aliyonayo.
“Kaamua Bi pili, pombe kujipikia na kilabuni kujiuzia pesa akipata, pesa msema kweli na NGUZO MAMA itasimama” (uk 14). Pia kujikomboa Kwa jamii kumejidhihirisha pale ambapo Bi moja na wenzake nao wakajiunga kuanzisha kiwanda cha kufuma mapambo ya nyumabani.
“……….katokea Bi moja, na lake jipya kiwanda kuanzisha, mapambo ya nyumbani kufuma, mapambo ukiyauza na pesa kujipatia, itakuaje NGUZO MAMA isisimame”. Uk 17.
Pamoja na uwezo wa wanawake wa kijiji cha patata, vile vile palikuwa na udhaifu ambao ulisababisha NGUZO MAMA kutosimama.
Mfumo dume ulikuwa ni udhaifu ambao ulisababisha maendeleo ya wanawake wa kijiji cha patata kutokuendelea. Kwa mfano katika kitabu hiki cha NGUZO MAMA tunamwona Bwana Sudi ambaye ni mume wa Bi pili anavyotumia mabavu katika kumnyanyasa mkewe. Hii imejidhihirisha katika uk 14-16
Sudi: (kwa Bi pili) haya nipe pesa ulizokwisha kupata.
Bi pili: Hee! Kwa nini nikupe?
Sudi: Lete pesa haraka kabla sijakukong’ota.
Udhaifu mwingine ni kupenda anasa na tamaa, mfano katika kitabu hiki cha NGUZO MAMA mhusika Bi moja ni mpenda anasa na mwenye tama. Katika tamaa yeye kwake kila toleo la Khanga anataka lisimpite. Uk 31-32 Bi moja anasema…
“Nakwenda babu wee meli hii isinikose, Bi moja ahaa jamani nitarudi lakini Khanga hizi zisinikose”
Vilevile udhaifu mwingine unajitokeza kwa Bi sita pale ambapo yeye alikuwa ni kahaba anayefanya ngono zembe na kuchukua mwanaume wa Bi tano. Kwa mfano uk. 35 Bi sita anaona kitu kwa mbali kwa Bi tano
Aisee hebu nishike kamba yangu mara moja. (upesi anaondoka, anasimama, anajikung’uta nguo na kujitengeneza vizuri halafu anatembea kikahaba polepole kama yuko matembezini. Mara anatokea Maganga Bi sita anamfuata, anachekeana. Maganga anamfanyia ishara amfuate. Bi tano anaona yanayofanyika, upesi anaacha kamba na kuwafuata)
Bi tano: Wee Bi sita, mshenzi unanichukulia mume wangu hivihivi kimachomacho. (Maganga anaondoka upesi upesi).
Msingi wa pili katika nadharia hii ni pamoja na kutazama matumaini ya binadamu katika kuyakabili magumu bila kukata tamaa.
Katika tamthiliya hii mwandishi anamwonesha Bi nane kama mfano wa wanawake katika jamii wenye ndoto na hali ya kuinua NGUZO MAMA ingawa wanapigwa vita na kutengwa ama kudhihakwa. Kwa mfano katika tamthiliya hii ukurasa wa 12 unasema…..
“……….Tena mwenyekiti mimi nilikuambia kuwa hao walimu hawampendi huyu Bi nane, yeye tu ndiye anayejiweka kimbelembele kama wanampenda, mbona walimu hao hao wanatoka kuja kuendeleza mipango yao?”. Pia wanawake wa kijiji cha Patata wana matumaini ya kuweza kuinua NGUZO MAMA siku moja licha ya changamoto mbalimbali wazipitiazo. (uk. 14.) inasema hivi,
“……Kaamua Bi Pili, pombe kujipikia, na kila kitu na NGUZO MAMA itasimama…..”
Bi nane anaonesha kutokukata tamaa licha ya kuona juhudi za kuinua NGUZO MAMA zinakwama katika harakati za kuinua NGUZO MAMA akisema.
Bi nane: “Tushirikishe wanaume pia. Nguzo mama itasiama kwani ina faida kwa wote, taifa na watoto wote. Faida kwa wote-wao taifa lote….”
Kutazama matumaini ya binadamu katika kuyakabili magumu hayo bila ya kukata tamaa (tumaini).
Wanawake wa kijiji cha Patata walitumaini kupata maendeleo yao binafsi na jamii nzima kwa ujumla kwa kufanya kazi mbalimbali ambazo zingeweza kuwaingizia kipato na kuachana na hali ya utegemezi kwa waume zao kazi hizo ni kama ushonaji, upikaji pombe na viwanda vidogo.
Kwa mfano ukurasa wa 12-17 Bi Pili anajishughulisha na upikaji wa pombe ili aweze kujikimu na majukumu ya nyumbani kwake.
Totolo: Lo!! Hata na wewe Bi Pili siku hizi unapika pombe, lo!
Shaba: Mwaka huu tutafaidi pombe. Kijiji kizima pombe.
Bi Pili: Eee ndio maendeleo mwaka huu tutainuka karibuni.
Vilevile anakuja Bi Moja na wazo lake jipya la kuanzisha kiwanda cha mapambo ya nyumbani.
Bi Moja: Kazi yetu inakwenda vizuri, vile vitambaa vilivyopelekwa kwenye maonesho tayari vimenunuliwa. Hata vile vya TTC navyo vimeshakwisha vyote.
Bi Moja: Je? Si niliwaambia mie kuwa tutapata.
Msingi wa tatu wa nadharia hii inajidhihirisha katika Tamthiliya ya NGUZO MAMA ni kuchunguza matatizo na furaha ambavyo vinaweza kusababishwa na makosa yaani kama vile wizi, mauaji, ndoa na magonjwa hata unyanyasaji.
Wizi, ndoa na unyanyasaji ni miongoni mwa matatizo ambayo mwandishi ameyadurusu katika Tamthiliya hii; Bado wanawake wa Patata wananyanyasika katika ndoa zao, wanaibiana wanaume pia hata manyanyaso ya kifamilia dhidi ya wanawake na yatima. Katika kitabu chetu ukurasa wa 43-44 unasema;
“……….Akalia Bi saba akalia, hana wa kumsaidia mume wake kafa na nduguze wamekuja juu, pesa wamechukua senti tano, vyombo na nguo zote walichukua wakagawana, roho ikampasuka Bi saba kuwaona hao ndugu walivyogombania mali wasiyoichuma.
“Kiti hiki changu, mie lile pembe langu, mie suruali hizi” Ilimradi kulikuwa zogo. (uk.36).
Katika msingi huu jamii nyingi za kiafrika wanawake wanaonekana kunyanyaswa au kugandamizwa na kudhalilishwa kwa kunyang’anywa mali walizochuma pindi waume zao wanapofariki. Kwa mfano ukurasa wa 39 tunaona Bi saba ananyang’anywa mali na watoto wake na shemeji zake.
Bi Saba: (Anaoneka kusikitika) Haa! Shemeji mmerudi kuchukua hata kitanda! Hata sufuria! Nitalala wapi na kupikia wapi jamani!
Kiando: Usitudanganye na kulia, onesha ulificha hela ama sivyo utaona cha mtema kuni.
Unyanyasaji mwingine tunaona bwana Sudi anamtukana mke wake mbele za watu na kumwambia;
……..Wee hawala zako ndio wanakutia jeuri unaninyima pesa. Toa pesa sasa hivi.
Pia upo unyanyasaji mwingine dhidi ya mwanamke ukurasa wa 53 kwani tunamwona mwanamke, Totolo akisema; Mie mke wangu alikuwa hajui kusema kwenda kwenye hiyo mikutano yao, akachonga ulimi.
Shaba: Wa kwangu mie nilimkong’ota nikampiga marufuku asiende tena.
Unyanyasaji mwingine wa akina mama ni kule kutelekezwa, kuachiwa mimba jambo linalosababisha kuwa na mzigo wa kulea watoto katika mazingira magumu kama inavyojidhihirisha ukurasa 4 chizi akionyesha shangazi yake;
Bi tatu: We chizi umefuata nini huku nyumbani kwangu. Hebu toka hapa tuna shughuli na wageni.
Chizi: Niende wapi? Kaka yako alinikana na wewe shangazi unanifukuza!
Maneno haya ya Chizi yanatudhihirishia kwamba mama yake alinyanyaswa na kutelekezwa na Baba yake.
Msingi wa nne ni kuangalia matatizo ya nafsi hasa katika kukata shauri au kuamua juu ya msimamo mgumu.
Matatizo ya nafsi yanaweza kusababisha maamuzi magumu katika jamii. Maamuzi yanaweza yakajenga au yasijenge. Katika kitabu cha NGUZO MAMA tunaangalia wahusika wengi wenye matatizo ya nafsi ambapo matatizo hayo husababisha maamuzi magumu katika jamii zao bila kujali athari au matokeo yatakayojitokeza. Kwa mfano ukurasa wa 21 inasema;
Mwenyekiti: Bi nane mimi nikiwa kama kiongozi wa kamati ya mashauri nakushauri kwa usalama wako urudi ukavunje hicho kikundi ulichounda kama mna jambo la kuzungumza basi mlipeleke kwa kiongozi wenu. Bi nne aliweka kwenye ajenda ya mikutano ya kawaida, hii tabia ya kuunda vikundi vidogo vidogo haikubaliwi.
Bi nane: Unaona mwenyekiti! Hii ni dharau! Nilikuambia bibi huyu ana dharau unaona!
Mwenyekiti: Bi nane, ukinyamaza ndio tukuelewe vipi. Mimi nakuomba nikiwa mwenyekiti wa kamati ya mashauri ujieleze kwa nini umefanya mambo haya.
Bi msimulizi: Bi nane macho kawakodolea,
kajisemea moyoni,
leo ntajionea
lipi litakalotokea.
Bi nane: Nieleze mwenyekiti naomba niambiwe shitaka langu. Nilichokosea ni nini au kuwa na madigrii au nini!
Mwenyekiti: Sikiliza Bi nane nimekueleza kuwa utoe maelezo kwa nini umeunda kikundi cha walimu watupu cha kupinga shughuli ya kusimamisha nguzo mama.
Bi nane: Basi kama hilo ndilo shitaka mimi nitatoa maelezo lakini naomba nitoe maelezo hayo kwa maandishi.
Bi nne: Unashindwa nini kusema hapa hapa, wewe si mwenyekiti wa kikundi chako, mwenyekiti kila wakati yuko tayari kujitetea sio mpaka aandike. Sio kutuletea tabia za kisomi hapa. (uk. 27-28).
Lakini pia matatizo ya nafsi yamejitokeza kwenye kitabu chetu hiki cha NGUZO MAMA katika ukurasa wa 40 ambao unasema hivi;
“Tabu taabu taabu
Watoto wangu hawana chakula
Watoto wangu wanashinda na njaa
Wanalala na njaa.
Msingi wa tano ni kuangalia kwa kina juu ya mgongano wa nafsi na mambo ya nje ya jamii.
Hii imejidhihirisha kwa mhusika Chizi ambaye alikuwa na mgogoro wa nafsi ambayo ilimuhuzunisha na kumfedhehesha
Chizi: Nani ana pendekezo?
Waoneni watu hawa
Hawapendi demokrasia
Nikisema yote haya mie
Wananiita mie chizi
Ambao macho mwakodoa
Kuwaacha wachache
Wanavyotaka kufanya………….uk. 32.
Pia Bi nane alikuwa na mgogoro wa nafsi pale alipopelekwa kwa mwenyekiti wa kijiji kujibu tuhuma zinazomkabili. Anawaza iwapo aendelee kushirikiana na wenzake au atengeneze maisha yake mwenyewe
HITIMISHO.
Kwa kuhitimisha nadharia ya saikochanganuzi imetumika kuhakiki tamthiliya ya NGUZO MAMA kwa kufuata misingi ya nadharia hiyo kwa kutumia wahusika wake katika kitabu hiki kama tunavyoona kwamba ina uhalisia wa jamii yetu ya kitanzania hususani hasa katika harakati mbalimbali zilizofanywa na jamii ya wanapatata zinazofanana kabisa na harakati zinazofanywa na wanawake wa kitanzania, mfano kuanzishwa kwa NGUZO MAMA katika jamii ya wanapatata kunasawiri uanzishwaji wa taasisi mbalimbali za kupigania ukombozi wa wanawake Tanzania (UWT) Chama cha uandishi wa habari cha wanawake Tanzania, (TAMWA) Chama cha madaktari wanawake Tanzania na vinginevyo. Hivi vyama vyote lengo kuu ni kupigania haki na ukombozi wa mwanamke dhidi ya ukandamizaji kwa mwanamke wa kitanzania na afrika kwa ujumla.
MAREJEO.
Martin E. A. (2005). Social science research conception, Methodology and Analysis. Makerere University.
Masamba. (2009). Kamusi ya Isimu, Falsafa ya Lugha: Dar es Salaam. TUKI Publishers.
Muhando, P. (2010). Nguzo mama: Nairobi-Kenya. Muwa Publishers ltd.
Sarantakos, S. (1997). Social research. (2nd Ed). Palgrave Publishers ltd
Comments