FAHAMU ELIMU YA TANZANIA BARA ILIVYOKUWA KABLA YA UHURU
Elimu ya Tanzania bara Kabla ya Uhuru
Elimu ya Jadi: Historia ya Elimu Tanzania Bara imegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni kabla na baada ya uhuru. Kabla ya kuja kwa wageni katika mwambao wa Tanganyika, kila kabila lilikuwa na mfumo wake wa elimu ya kijadi. Elimu ya Kijadi ilitokana na taratibu za kila siku za jamii za makabila mbalimbali. Elimu hiyo iliyojumuisha maarifa, stadi, maadili, utamaduni, mbinu na taratibu nzuri za kufanya kazi na kujilinda kutokana na mabaa ya njaa, magonjwa na maadui wa usalama wa jamii na wa mali zao ilirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mambo ya kujifunza yaligawanyika kirika na kutolewa na watu wazima nyumbani, kazini na katika nyanja nyingine za maisha. Mfumo huu ulianza kuwa na mabadiliko katika malengo na utoaji wake tangu wakoloni walipoingia nchini.
Elimu Wakati wa Ukoloni: Wageni wa kwanza Tanzania Bara walikuwa Waarabu, wakifuatiwa na Wareno, Wajerumani na Waingereza. Kwa kuwa wageni hao walipokezana madaraka ya sehemu ya nchi au nchi nzima, kila kundi lilibadili mfumo wa elimu kulingana na matakwa yao bila kujali yale yaliyokuwa na manufaa kwa Watanzania Bara. Shule za mataifa mbalimbali zilitofautiana katika malengo, mitaala, sifa na taaluma za walimu, lugha ya kufundishia, na ubora wa majengo ya shule na nyumba za walimu.
Waarabu walipoingia walianzisha mafunzo ya Quran. Elimu hii ilitia mkazo uenezi wa dini ya Kiislamu na Utamaduni wa Kiarabu. Utawala wa Kijerumani na Kiingereza ulitanguliwa na ujio wa Wamisionari. Walipofika, Wamisionari walitoa elimu kufuatana na imani yao na historia ya nchi walikotoka. Elimu ya Wamisionari ilisisitiza uenezi wa dini ya Kikristo. Utawala wa Kijerumani ulitoa elimu iliyotilia mkazo stadi, maarifa na mafunzo ya kazi na uraia mwema kwa Serikali ya Ujerumani. Mfumo wa elimu ya Waingereza katika Tanzania Bara ulikuwa na misingi ya ubaguzi wa rangi na ulitoa nafasi na nyenzo bora zaidi za elimu kwa watoto wa Kizungu na Kiasia kuliko Waafrika. Lengo kubwa la elimu lilikuwa ni kupata watumishi Waafrika ambao wangetumika katika kutetea matakwa ya wakoloni, na hivyo kuwafanya wasomi kuwa tegemezi
Comments