ISHU YA VYETI FEKI IMEICHUKUA SURA MPYA TENA

Watumishi wa umma wafikia 10,000, Wamo mabalozi, wakuu wa wilaya, mikoa Na Fredy Azzah-DODOMA SEKESEKE la watumishi wa umma kushughi vyeti vya elimu limezidi kuchukua sura mpya na sasa wamefikia zaidi ya 10,000. Hatua hiyo, inatokana na uhakiki uliofanywa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ambayo imebaini waombaji kazi 39,511 kati yao, 1,951 wana vyeti vya kughushi. Kuongezeka kwa idadi hiyo, kunatokana na kauli ya Rais Dk. John Magufuli, wiki iliyopita, kwamba anasubiri ripoti ya wafanyakazi wa Serikali ambao wamebainika kuwa na vyeti feki. Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam, wakati akizindua mabweni mapya ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Alisema anafahamu idadi ya watumishi wenye vyeti feki ni zaidi ya 9,000 na anaisubiri ripoti hiyo kuifanyia kazi. “Kwa hiyo mnaweza mkaona shida zilizopo katika nchi hii, huku wafanyakazi hewa karibu 19,000, wanafunzi hewa ni zaidi ya 56,000, kila mahali unapokwenda ni matatizo, lakini ni lazima niyatatue matatizo kwa sababu mlinichagua kwa ajili hiyo,” alisema Rais Magufuli. Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2017/18 kwa ofisi yake jana bungeni mjini hapa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema baada ya kubainika kwa hali hiyo, wahusika waliondolewa kwenye mchakato, huku vyeti hivyo vikiwasilishwa katika mamlaka husika kwa hatua za kisheria. “Wahusika waliondolewa katika mchakato pamoja na vyeti hivyo kuchukuliwa na kuwasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema Kairuki. Hata hivyo, zipo taarifa zinazodai kuwa orodha ya watumishi wa umma ambao wamebainika kuwa na vyeti feki itawekwa hadharani Aprili 30. Zaidi inaelezwa kuwa sakata hilo la vyeti feki linawagusa pia mabalozi ambao ni wawakilishi wa Watanzania katika mataifa mbalimbali, wakuu wa wilaya na mikoa.   TAKUKURU YAOKOA MABILIONI Aidha, Waziri Kairuki, alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imefanikiwa  kuokoa zaidi ya Sh bilioni 12,  kutokana na operesheni mbalimbali ilizofanya katika kipindi cha kuanzia Julai, mwaka jana hadi Machi, mwaka huu. Akitoa mchanganuo wa fedha hizo, alisema Sh bilioni 8.009 zilitokana na ukwepaji ushuru kupitia mashine za kielektroniki (EFDs), Sh bilioni 2.6 zilitokana na ubadhirifu, Sh milioni 912.396 mishahara hewa na Sh milioni 794.182 ziliokolewa kutoka maeneo mengine. “Nguvu kubwa imeelekezwa kudhibiti rushwa katika eneo la ukusanyaji mapato ya Serikali, uzuiaji wa malipo hewa na ukaguzi wa miradi ya maendeleo,” alisema Kairuki.   MALI ZATAIFISHWA Alisema pia kutokana na kuimarika kwa kitengo cha ufuatiliaji na urejeshaji wa mali, Takukuru imefanikiwa kutaifisha nyumba sita ambazo tano zipo Buhongwa na moja Ilelemela jijini Mwanza. Kairuki alisema Takukuru pia imetaifisha magari manne, yakiwamo mawili aina ya Totoya Chaser, Toyota Land Cruiser moja na Mitsubishi Fuso moja, ambayo yote yalipatikana kwa rushwa. Alisema pia katika kipindi hicho cha Julai 2016 hadi Machi 2017, uchunguzi wa majalada 376 ulikamilika na kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kupata kibali cha kufikisha watuhumiwa mahakamani. Yaliyopata kibali ni 157. Pia kesi 706 ziliendeshwa mahakamani zikiwapo 227 mpya, 264 ziliamuliwa na mahakama, 161 watuhumiwa wake waliachiwa huru na 103 watuhumiwa wake walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo ama kulipa faini. Alisema kesi 33 ziliondolewa mahakamani kwa sababu mbalimbali, huku 409 nyingine zikiwa zinaendelea kusikilizwa.   VIBALI VYA AJIRA Waziri Kairuki alisema kati ya Julai 2016/17, vibali vya ajira mpya kwa nafasi 9,721 vimetolewa kwa waajiri, vikijumuisha nafasi 3,174 kwa Jeshi la Polisi, 1,000 Jeshi la Magereza, 952 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, 297 Jeshi la Uhamiaji na 50 wataalamu wa afya Hospitali ya Mloganzila. Vibali vingine vya ajira vilivyotolewa ni vya walimu wa masomo ya sayansi na hisabati 4,129 na nafasi 219 za mafundi sanifu wa maabara za shule. Alisema pia katika kipindi hicho, watumishi 19,708 wameondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara.   UKATA Kwa mujibu wa hotuba hiyo ya Kairuki, hadi sasa kiasi cha fedha kilichotolewa na hazina ni kidogo ikilinganishwa na kilichoidhinishwa na Bunge. Katika mwaka wa fedha 2016/17, Ofisi ya Rais Ikulu, iliidhinishiwa na Bunge Sh bilioni 14.962 kwa matumizi ya kawaida, lakini hadi kufikia Machi 2017, kiasi kilichotolewa ni Sh bilioni 11.063. Alisema kwa upande wa Ofisi ya Rais na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri na taasisi zilizo chini ya Ikulu, ziliidhinishiwa Sh bilioni 793.164 na kati yake Sh bilioni 362.715 ni kwa matumizi ya kawaida na Sh bilioni 430.449 za maendeleo. Hadi kufikia Machi mwaka huu, Sh bilioni 547.583 zilipokewa na kutumiwa, kati yake Sh bilioni 260.648 matumizi ya kawaida na Sh bilioni 286.934 ni za maendeleo. Licha ya kutotekelezwa kwa bajeti hiyo kwa mwaka 2017/18, wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa na Bunge Sh bilioni 821.322 kwa Ofisi ya Rais, kati yake Sh bilioni 430.351 ni matumizi ya kawaida na Sh bilioni 390.970 ni miradi ya maendeleo.

Comments

Popular posts from this blog

Kwa kutumia mifano jadili istilahi muhimu katika tamthiliya ya tanzia.

ZIFAHAMU METHALI ZA KISWAHILI ZIPATAZO 600 NA ZAIDI

Uhakiki wa tamthiliya ya nguzo mama kwa kutumia nadharia ya saikochanganuzi