Mgogoro wa CUF Ulivyoibua Mvurugano Katika Uchaguzi wa Wabunge ELA
Wakati wabunge saba kati ya tisa watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (Eala) wakipatikana juzi usiku, suala la wawakilishi wa upinzani limetawaliwa na hali ya kutoeleweka, huku ikibainika rasmi kuwepo kwa CUF “A” na CUF “B”.
Kikao cha juzi kilichotawaliwa na mjadala wa kikanuni kuhusu wawakilishi wa Chadema na CUF, kiliweka rekodi ya kuchukua muda mrefu baada ya kumalizika saa 7:00 usiku kikikipiku kikao kilichojadili sakata la uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Bunge lilichagua wanachama sita wa CCM kuingia Bunge la Afrika Mashariki, pamoja na mmoja kutoka CUF, ambaye amezua mjadala baada ya jina lake kukubaliwa na msimamizi wa uchaguzi licha ya kusainiwa na naibu katibu mkuu wa chama hicho badala ya katibu mkuu ambaye aliwasilisha jina jingine.
Waliopitishwa ni Fancy Nkuhi, Happines Legiko, Maryam Ussi Yahya, Dk Abdullah Makame, Dk Ngawaru Maghembe na Alhaj Adam Kimbisa kutoka CCM, wakati Habib Mnyaa, aliyekuwa amevuliwa uanachama na CUF, alichaguliwa pia kuingia kwenye chombo hicho.
Hata hivyo, wanachama wawili walioteuliwa na Chadema kuwania ubunge wa Eala, Ezekiah Wenje, aliyepata kura 124 za ndiyo na 174 za hapana, na Lawrence Masha, aliyepata kura 124 za ndiyo na 198 za hapana, hawajaingia kwenye chombo hicho, kitu ambacho kimeifanya Chadema kuamua kwenda mahakamani.
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema jana kuwa uchaguzi huo ulikuwa ni batili kutokana na taratibu kutofuatwa.
Pia, hoja ya kuwepo kwa CUF A na B iliyozungumziwa na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi huo imeibua mvurugano kwa chama hicho ambacho kimekuwa na mgogoro na mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba tangu alipojiuzulu mwaka juzi na kujirejesha mwaka jana.
CUF na pande mbili
Katika uchaguzi huo uliofanyika bungeni mjini Dodoma, CUF ilipeleka wagombea wanne baada ya upande wa Profesa Lipumba kutuma majina matatu huku upande wa Maalim Seif ukipeleka jina moja.
Majina yaliyopelekwa na upande wa Profesa Lipumba ni Mnyaa, Thomas Malima na Sonia Magogo huku upande wa Maalim Seif ukipeleka jina la Twaha Taslima.
Kitendo cha Dk Kashililah kutangaza kukubali majina ya pande zote mbili, kilifanya wabunge waanze kuhoji sababu za ofisi ya Bunge kukubali kupokea majina ambayo hayajasainiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Akihoji suala hilo, Lissu alisoma barua ambayo ofisi ya Bunge ilimwandikia Maalim Seif kuthibitisha kupokea jina la Taslima na kuandika kasoro ambazo zilionekana katika fomu, akisema huo ni uthibitisho kuwa Maalim Seif ndiye katibu wa chama hicho.
Alihoji sababu za kupokea fomu za upande mwingine wakati Maalim Seif yupo. Spika John Ndugai alisema hana taarifa za mawasiliano hayo na hivyo kumtaka katibu atoe maelezo.
“Nafikiri anachokisoma (Lissu) ni sahihi na tuliandika. Msingi wa andiko letu ulitokana na barua ya tarehe 28 Machi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi,”alisema Dk Kashililah wakati akitoa maelezo.
“Hatukuviandikia vyama kuviomba, tulitoa GN 376, vyama viliandika vikaomba. Mimi sikuvitambua, aliyevitambua vyama ni mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Ninayo orodha ya CUF “A” wamewasilisha kupitia kwa naibu katibu mkuu, na CUF “B” kupitia kwa katibu mkuu.
“Mheshimiwa Spika ni vizuri tuelewane. Katika barua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndipo viongozi wawili wa CUF wanapokutana na wala si ofisi ya msimamizi wa uchaguzi.
"Mimi nieleze wazi. Kwani aliyepeleka jina la Mnyaa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni nani? Na aliyepeleka jina la Taslima ni nani? Sasa mbona wote wameleta?”
Hivi karibuni Profesa Lipumba alitangaza kumteua Sakaya kukaimu nafasi hiyo, akisema Maalim Seif hatii maagizo. Kwa mujibu wa katiba ya CUF, katibu mkuu huchaguliwa na mkutano mkuu wa chama.
Akieleza utaratibu wa kuwathibitisha wagombea wa Eala, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Nec, Ramadhani Kailima alisema walipokea majina ya wagombea kutoka vyama vya siasa na kwa suala la CUF hawajui kuhusu mgogoro unaoendelea.
“Sisi hatupitishi majina ya wag- ombea. Soma taarifa ya Spika kwenye GN (Gazeti la Serikali). Kazi yetu ni kuthibitisha wagombea. Mimi sijui kama kuna mgogoro CUF. Tena andika kwa wino mweusi kabisa,” alisema Kailima.
“Sifa ya mtu kugombea ubunge ni lazima atokane na chama cha siasa na ni lazima awe raia wa Tanzania. Sasa kama amedhaminiwa na Maalim Seif au Lipumba, sisi hatujui kama kuna mgogoro.
“Mwenye jukumu la kusajili chama ni Msajili wa Vyama vya Siasa na akishasajili anawasiliana na taasisi nyingine. Kwa hiyo sisi tunaangalia uongozi alioutambua. Nec inaangalia sifa ya mtu kuwa mbunge, vyama vya siasa kama CCM, CUF Chadema ndiyo wanatuletea majina,” alisema Kailima.
Alipoulizwa kuhusu katibu aliyetakiwa kutia saini za wagombea wa CUF, Kailima alisema Nec haifungwi na mgogoro uliopo.
“Tume haifungwi, tunawasiliana na mwenyekiti au katibu. Mwenyekiti wa chama anawasiliana na mwenyekiti wa Tume na katibu mkuu anawasiliana na mkurugenzi wa uchaguzi,” alisema.
“Ninyi si mliandika kuwa Magdalena Sakaya ameteuliwa kuwa kaimu katibu mkuu wa CUF na msajili akaridhia? Sisi tunawasiliana na huyo huyo pia.
“Lipumba anawasiliana na mwenyekiti wa Tume na Maalim Seif anawasiliana na mimi mkurugenzi.”
Akizungumzia kuhusu wagombea watatu wa CUF, Sakaya ambaye pia ni mbunge wa Kaliua, alisema alitia saini fomu zao kama kaimu katibu mkuu.
“Majina yalipelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuthibitishwa kisha yakapelekwa Idara ya Uhamiaji kuthibitisha uraia ndipo yakapelekwa kwa katibu wa Bunge,” alisema Sakaya.
“Fomu zao nilitia saini mimi kama kaimu katibu mkuu kwa sababu katiba yetu inasema kama katibu mkuu hayupo, nafasi yake inakaimiwa na naibu katibu mkuu.”
Comments