ZITO KABWE AGONGA MWAMBA
Zitto Kabwe Agonga Mwamba Ubunge ELA....... Spika Ndugai Agomea Maombi Yake
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amegonga mwamba baada ya Kamati ya Kanuni ya Bunge kutoa msimamo wake kuhusu uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Hatua hiyo inatokana na Zitto kuwasilisha barua kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, Machi 28, mwaka huu akitaka kamati hiyo kutoa ufafanuzi wa mgombe wa kundi C ili kila chama kiweze kushiriki uchaguzi, badala ya kupewa kwa vyama vilivyokuwa na idadi kubwa ya wabunge.
Kutokana na Tangazo la Bunge kwenye gazeti namba 11 la Machi 17, lililotangaza uchaguzi huo na masharti yake, Zitto, alisema mwongozo wa uchaguzi huo unavunja kanuni mbalimbali na kwamba kitakachofanyika sasa kitakuwa ni uteuzi na si uchaguzi.
Alisema pia mwongozo huo, mbali na kuvunja mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotaka suala la jinsi lizingatiwe kwenye wabunge wanaokwenda kuiwakilisha nchi katika Bunge hilo, lakini pia inavinyima vyama vingine vyenye uwakilishi bungeni haki ya kuchaguliwa.
Chanzo cha kuaminika kimeema kuwa uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Kanuni, kilichokutana juzi mjini Dodoma chini ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, huku Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson akihudhuria.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.
Wengine ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe pamoja na wajumbe kadhaa, ambapo baada ya kufunguliwa kwa kikao hicho kilichomalizika usiku wa juzi, Spika Ndugai, alihoji uhalali wa Zitto kuandika barua ya kuhoji mgawanyo huo wa wabunge wa EALA.
“Kifupi ni kwamba Zitto amekwama na hana tena namna maana Spika alimsema sana kutokana na mgawanyo lakini kabla ya kuendelea zaidi kwamba alimuuliza Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Kabudi kama kuna tatizo naye akasema hakuna na Spika hajakosea.
“… ila ni kikao ambacho Spika kwa kweli amesimamia sheria na ni kiongozi asiyeyumba katika kusimamia sheria, sasa tunakwenda kwenye uchaguzi huku ukweli ukiwa umeshajulikana, CCM watakuwa na viti sita, Chadema viwili na CUF kimoja,” alisema mtoa habari huyo
Baaada ya majadiliano ya kina na ufafanuzi wa kisheria kuhusu mgawanyo huo wajumbe wa Kamati ya Kanuni walikubaliana na Spika Ndugai kwa kauli moja, huku hoja ya Zitto ikitupwa na uchaguzi huo wa EALA utafanyika kwa kuzingatia uwiano wa idadi ya wabunge wa vyama vyenye uwakilishi bungeni.
Hata hivyo kanuni ya 5(5) ya nyongeza ya tatu ya kanuni za Bunge inaeleza “Chama chochote cha siasa chenye haki ya kusimamisha mgombea wa EALA kinaweza kuweka wagombea watatu katika ya wagombea ubunge”.
Kutokana na hilo msingi huo wa kikanuni inaonesha kuwa vyama vingine tofauti na Chadema , CUF na CCM, haviwezi kusimamisha wagombea kwa sababu havikidhi kigezo cha kanuni ya 12 za Kudumu za Bunge.
Comments