Serikali yatoa ahadi
Serikali yaahidi kuzifanyia kazi changamoto za Kikao cha Wadau
-------------------------------------------------
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe amesema Serikali itahakikisha inatekeleza maazimio yote yaliyopitishwa kwenye Mkutano wa pamoja wa mwaka wa Wadau wa Elimu uliofanyika kwa siku nne mjini Dodoma.
Mhandisi Iyombe ameyasema hayo wakati akifunga Mkutano wa mwaka wa wadau wa Elimu wenye lengo la kujadili changamoto, mafanikio ya Elimu na kuona namna gani kama wadau wanaweza kutafuta njia ya pamoja ya kuboresha Mfumo wa utoaji wa Elimu Tanzania.
�Nimepokea maazimio yote ya Mkutano huu na nitayawasilisha panapohusika kwa ajili ya utekelezaji lakini pia niwapongeze kwa kazi kubwa mliyoifanya, kuanzia wataalam kutoka Serikalini, sekta binafsi, Mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau wa Elimu hakika mmefanya kazi kubwa na kupitia Mkutano huu tutaona mabadiliko makubwa katika Sekta hii ya Elimu� alisema Iyombe.
Akitoa salamu za Wizara Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu. Sayansi na Teknolojia Prof Sylvia Temu amesema kikao cha Wadau wa Elimu kimekuwa na tija kwa kuwa pamoja na mambo mengine kimejadili masuala yanayotokana na utafiti wa elimu na kwamba matokeo ya tafiti yaliyoonyesha changamoto yatafanyiwa kazi kwa pamoja kati ya Serikali, Wadau wa Maendeleo na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu Bw. Tixon Nzunda amesema mojawapo ya maazimio na malengo ni kuhakikisha mifumo yote ya elimu inakuwa elimu jumuishi na Serikali kuhuisha mipango ya elimu iliyopitishwa ambayo itatekelezwa ndani ya miaka mitano.
�moja ya maazimio na makubaliano yaliyofikiwa ni kuhakikisha kwamba Serikali inahuisha mipango yake yote na Wadau wote wa Elimu kuahakikisha kwamba utekelezaji unaelekezwa kwenye Mpango wa kuboresha Sekta ya Elimu kwa miaka mitano ambao umekwisha pitishwa, mifumo yote inayohusu masuala ya elimu kwa maana ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari, Elimu ya juu, pamoja na Elimu Maalum inakuwa elimu jumuishi kwa maana ya kwamba inahakikisha haimuachi motto yeyote nje ya Mfumo�, alisema Nzunda.
Kwa kuhitimisha mahojiano na Wanahabari, Naibu Katibu Mkuu alisema lengo la jumla katika kikao hicho cha Wadau ni kwenda kutekeleza Mpango wa Elimu wa miaka mitano kuanzia mwaka 2017/18 hadi 2021/22 na kuanzisha kampeni ya kitaifa juu ya suala la elimu jumuishi kwa kuwa suala hili ni la wote na sio Serikali pekee lakini pia kuhakikisha tafiti zote za elimu zinafanyiwa kazi ili kuleta matokeo makubwa katika Sekta ya Elimu nchini.
Kikao cha Wadau wa Elimu na Serikali hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuboresha Sekta ya Elimu iliyopana zaidi na changamoto nyingi ambazo zimetatuliwa kwa kiwango kikubwa na Serikali. Aidha,kikao hiki cha siku nne kwa mwaka huu kimekuwa na tija kutokana na washiriki karibu wote kuhudhuria na kushiriki ipasavyo kwa kuchangia hoja.
Comments